Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Habari ya Shirika la Habari la Hawza, habari ifuatayo ni simulizi fupi iliyonukuliwa kutoka katika ripoti ya Raed Musa, mwanahabari na mwanaharakati wa vyombo vya habari wa Kiarabu, kuhusu juhudi za mwalimu mmoja wa Kipalestina za kuendeleza elimu kwa watoto wa Ghaza katikati ya magofu yaliyoachwa na vita.
Huko Gaza, ambako vita vimeharibu shule nyingi, bado wapo walimu ambao hawataki mwanga wa elimu uzimwe.
Mahmoud Hamad, mwalimu wa Kipalestina, licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi, hajaukimbia wala kuuacha wajibu wake wa kufundisha. Anakusanya wanafunzi wake katika maeneo ya wazi, chini ya vivuli vya miti na katika nyua za shule zilizoharibiwa, ili waweze kuendelea na masomo yao.
Hapa, hakuna tena madarasa yenye vifaa vya kisasa wala huduma za kawaida zinazopatikana shuleni. Hata hivyo, mwalimu huyu ameamua kuendelea kufundisha watoto, huku akiwaonyesha kwamba hata katika mazingira magumu zaidi, bado inawezekana kufikiria na kupanga mustakabali.
Kinacholifanya darasa hili rahisi kuwa na athari kubwa ni ndoto za watoto ambao, licha ya kuishi katikati ya magofu, bado wana matumaini na ndoto kuhusu maisha yao ya baadaye.
Muatasim, mwanafunzi mwenye umri wa miaka saba, anatamani kuwa mhandisi ili aweze kujenga upya viwanda vya Ghaza vilivyoharibiwa, Sama anatamani kuwa daktari ili aweze kuwasaidia waliojeruhiwa, huku Joud, mwenye umri wa miaka tisa, akitamani kuwa mwalimu ili siku moja naye aweze kuwafundisha watoto wengine.
Watoto hawa wanakabiliwa na uhaba wa vifaa na nyenzo za kujifunzia, na wengi wao wamepitia siku na nyakati ngumu sana. Hata hivyo, bado hawajaziacha ndoto zao. Kwao, kusoma si suala la kujifunza maneno na namba chache tu; bali ni njia ya kufikia mustakabali bora zaidi.
Mahmoud Hamad, kwa kuendesha masomo katikati ya magofu, pia anaonyesha kwamba elimu haiwezi kufungwa ndani ya kuta na majengo pekee. Huenda leo watoto hawa hawakai kwenye madawati ya kawaida ya shule, lakini bado wanaweza kuota ndoto ya kujenga hospitali, shule na viwanda.
Huko Ghaza, shule zimeharibiwa, lakini ndoto za watoto bado ziko hai. Na bado wapo walimu ambao hawaruhusu matumaini ya kuwa na mustakabali bora yazikwe chini ya vifusi vya vita.
Chanzo: Ripoti ya Al Jazeera.
Maoni yako